Write your own article idiot!
error: Content is protected !!

Monday, June 25, 2018

KISWAHILI: FORM FOUR: Topic 5 - UANDISHI

 Join Our Groups

TELEGRAM | WHATSAPP


Schemes of Work 2024


English Course - Free


Kenya Resources








TOPIC 5: UANDISHI

UANDISHI WA INSHA ZA KIADA

Insha ni kifungu cha maandishi kilichoandikwa kutokana na mtazamo wa mwandishi katika kujadili juu ya mada fulani. Mwandishi anaweza kuandika kuipinga mada hiyo au kuishadidia mada hiyo. Kuna aina mbili za insha, insha za kaida (zisizo za kisanaa) na insha za kisanaa.

Insha za kaida ni insha zinazotumia lugha ya kawaida kuelezea mambo mbalimbali katika jamii, mfano juu ya mazingira, uchumi, biashara, historia n.k.


Muundo wa Insha za Kaida

 Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:

1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k

2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.

3. Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.

4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.


Mambo ya Kuzingatia katika Uandishi wa Insha

Taratibu za uandishi zinapozingatiwa insha pia itasomeka vizuri na pia itakuwa na mtiririko mzuri wa mawazo.

1. Epuka kutumia vifupisho vya maneno visivyo rasmi. 
Uandishi wa insha ni suala rasmi, kwa hiyo katika uandishi wake inatakiwa kuzingatia kuepuka kutumia vifupisho ambavyo sio majumui yaani havijulikani. Kwa mfano maandishi kama, xamahani (samahani), ckatai (sikatai) na mengine yafananayo kama hayo ni lazima yaepukwe katika uandishi wa insha.

2. Andika utangulizi unaovuta umakini wa msomaji. 
Hiki ni kipangele cha muhimu sana, msomaji anapoona kwamba kwenye utangulizi hakuna kitu kinachomvutia hataendelea kuhangaika kusoma insha hiyo.

3. Andika kiini cha insha kwa mpangilio mzuri.          
Unatakiwa kuandika insha yako katika mpangilio mzuri huku kila wazo kuu likipewa aya yake na kuwepo na mtiririko mzuri wa mawazo.

4. Andika hitimisho la insha likiwa linahitimisha mawazo yaliyokwishajadiliwa katika kiini. Hakikisha unapofanya hitimisho epuka kudokeza wazo jipya ambalo linazua mjadala mpya, hakikisha hitimisho lako linabeba mawazo uliyokwisha yajadili katika insha yako na wala yasiwe mawazo yanayotoka nje ya kile ulichokijadili.

Kuandika Insha


UANDISHI WA HOTUBA

Hotuba ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani. Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi halisi na mwandishi hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake. Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika fulani, daktari, n.k. Hadhira katika hotuba husheheni wageni waalikwa, wanachama, wafuasi, wananchi, n.k ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa katika hotuba hiyo.


Muundo wa Hotuba

Hutuba inakuwa na muundo ufuatao:
Anwani
Anwani, mada au kichwa cha hotuba hurejelea mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja hadhira.
  • Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa wananchi.
  • Hotuba ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi
Utangulizi
  • Anza hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano (hadhira).
  • Wataje kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina pekee kunatosha.
  • Jitambulishe kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia hadhira isiyokujua au wageni.
  • Tanguliza mada yako.

Kwa mfano:
Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Mbunge, wanachama wa kikundi hiki cha Mazingira, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi cha Mazingira na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa …

Kiini
  • Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho
  • Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.
Tamati
  • Hakikisha kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
  • Unaweza kumaliza kwa shukurani


UANDISHI WA RISALA

Risala ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu hasa hasa wanafunzi, wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi n.k ili kutoa maelezo ya haja zao mbalimbali na mahitaji yao au kuonyesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi.


Muundo wa Risala

Utanguizi
  • Cheo cha kiongozi anayehusika
  • Kundi linalowakilishwa
Kiini
  • Maelezo ya hali halisi ya maswala na msimamo wa kundi linalowakilishwa.
  • Mapendekezso na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Hitimisho
  • Shukrani
Tanbihi: Kama vilivyosemwa awali risala ni hotuba fupi lakini inachukua mambo muhimu tu na kuyaeleza. Hivyo risala yenyewe huwa ni maelezo ya muhtasari kwa jambo linalohitaji maelezo marefu Katika hotuba. Utungaji wa risala unahitaji uangalifu sana na lugha ya heshima iliyo wazi kueleweka kwa kiongozi.


Mfano wa Risala:

Ndugu Mgeni rasmi, Walimu, Wanafunzi wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha nne, tunayo heshima na furaha kubwa , kukukaribisha ili ushiriki nasi katika siku hii muhimu na kusikia mafanikio mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo yetu hapa shuleni.

Shukrani zetu za pekee na za dhati ziende kwa uongozi mzima wa Shule na walimu wetu wote kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema; kwasababu tupo tofauti sana na tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.

Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60. Mpaka leo tunapohitimu tupo wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43, na wasichana 47. Wengine wameshindwa kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema wa Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii tunahitimu kidato cha nne.

Ndugu mgeni rasmi, elimu hii ya kidato cha nne imetupatia msingi mzuri wa kujiunga na Elimu ya juu, pia imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri, kufanya kazi vizuri na kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha sisi wanafunzi kupata elimu ya mambo mbalimbali kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano; tumepata elimu ya uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia kwa ujumla, pia tumeweza kupata uelewa kuhusu afya na magonjwa, usalama katika mazingira yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu, na viwanda. Vilevile tumeelewa umuhimu wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata ujuzi wa kuinua uchumi wetu wa taifa.

Ndugu mgeni rasmi, mafanikio hayo yamepatikana kwasababu ya ushirikiano mzuri kati yetu na walimu wetu. Tangu tujiunge na shule hii tukiwa kidato cha kwanza tumefanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara jambo lililo tusaidia kuinua taaluma yetu.Tunawashukuru sana walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri katika mitihani yetu ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki sana.

Ndugu mgeni rasmi, tumepata changamoto mbalimbali wakati wa maisha yetu ya kielimu hapa shuleni, kama ifuatavyo;

Ndugu mgeni rasmi, tuna changamoto ya upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea kushindwa kujisomea vizuri, kwani kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya ishirini (20).

Ndugu mgeni rasmi, changamoto nyingine ni upungufu wa vifaa vya maabara, hii inapelekea kuchangia kifaa kimoja, hivyo tuna tumia muda mwingi sana kujifunza na kumuelewa mwalimu.

Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi; hii imepelekea kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.

Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa samani za shule, kama vile; madawati kwa ajili ya wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya walimu; hii imepelekea baadhi ya wanafunzi wenzetu kukaa wawili kwenye dawati moja.

Ndugu mgeni rasmi, maji ni changamoto hapa shuleni, kwani shule haina kisima cha maji, hii imepelekea shule kununua maji kwa gharama kubwa, ambayo hayatoshelezi mahitaji ya shule, kama vile usafi; hususani kwa upande wa vyoo, bila kuwa na maji ya kutosha tutapata magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu.

Ndugu mgeni rasmi, changamoto ya vifaa vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni afya, shule yetu ina upungufu mkubwa wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya miguu, pete na mikono, pia hatuna milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya viwanja vya michezo yote tunayocheza hapa shuleni.

Ndugu mgeni rasmi, tunashukuru uongozi wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo ya sayansi; shule imeweza kutenga chumba kimoja cha darasa kitumike kama maabara japo kuwa kuna upungufu mkubwa wa vifaa.

Ndugu mgeni rasmi, tunayo matumaini kwamba maombi yetu umeyasikiliza na utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe unaweza kupitia Hlimashauri unayo isimamia, asante sana.

Mwisho tunaomba msamaha wa dhati toka moyoni mwetu kwa Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi pale tulipoenda kinyume na matazamio yenu, kwani watu wakiishi pamoja tofauti lazima ziwepo, tunatumaini mtapokea msamaha wetu, nasi hatuna jambo lolote baya kwenu.

Ndugu mgeni rasmi, tuna kushukuru sana kwa kufika katika Mahafali yetu, kwani tunatambua kuwa unamajukumu mengi ambayo umeyaacha na kuwepo hapa kwaajili yetu.
  
Kuandika Risala


UANDISHI WA KUMBUKUMBU ZA MIKUTANO

Kumbukumbu za mikutano ni rekodi zinazowekwa na katibu wa mkutano wakati mkutano unapoendelea ili kuhifadhi yanayojadiliwa na kukubaliana katika mkutano huo. Katibu anapaswa kufuatilia mtindo maalum wa kuandika kumbukumbu hizo kulingana na mpangilio katika mkutano.


Mambo ya Kuzingatia katika Uchukuaji wa Kumbukumbu za Mikutano

Mambo ya kuzingatia katika uandishi wa kumbukumbu ni kama yafuatayo:

1. Kichwa cha kumbukumbu – Kichwa cha kumbukumbu kinapaswa kutaja mambo yafuatayo: Ni mkutano wa akina nani? Unaandaliwa wapi? Unaandaliwa lini? Unaanza saa ngapi? Mfano wa Kichwa cha Kumbukumbu: Kumbukumbu za Mkutano wa Shirika la Msalaba Mwekundu Shuleni ulioandaliwa tarehe saba Agosti 2001 katika Ukumbi wa Mikutano kuanzia saa Tisa alasiri.

2. Waliohudhuria – Andika orodha ya wote waliofika kwenye mkutano huku kuanzia na yule mwenye cheo cha juu zaidi hadi kwa wanachama. Pia onyesha vyeo vyao.

3. Waliotoa Udhuru -Hawa ni wale walioomba ruhusa kutohudhuria mkutano

4. Waliokosa kuhudhuria - Hawa ni waliokosa kuhudhuria mkutano, bila kutoa udhuru)

5. Waalikwa - Hawa ni wageni walioalikwa katika mkutano, k.v mlezi wa chama, afisa wa kiutawala, n.k)

6. Ajenda -orodhesha hoja zitakazorejelewa katika mkutano huo


Kumbukumbu   
       
KUMB 1
Kumbukumbu ya kwanza huwa ni kufunguliwa kwa mkutano na ujumbe kutoka kwa mwenyekiti.
KUMB 2
Kusomwa kwa kumbukumbu za mkutano uliotangulia na kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo kwa kutiwa saini.
KUMB 3
Maswala yanayoibuka kutokana na kumbu kumbu zilizosomwa. (Kumbuka kutaja nambari ya kumbu kumbu hizo)
KUMB kuendelea
Maswala katika ajenda
KUMB ya Mwisho
Maswala mengineyo yasiyokuwa kwenye orodha ya ajenda.
Tamati
Kufungwa kwa mkutano. Taja mkutano ulifungwa saa ngapi; mkutano ujao utakuwa tarehe ngapi; kisha acha nafasi ya kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo katika mkutano utakaofuatia.

Mfano:
KUMBUKUMBU ZA MKUTANO WA CHAMA CHA KISWAHILI ULIOANDALIWA KATIKA CHUMBA CHA MIJADALA TAREHE 24 JUNE 2013 KUANZIA SAA TATU ASUBUHI

Waliohudhuria
  1. Teddy Mbogela – Mwenyekiti
  2. Vaileth Matiko – Mweka hazina
  3. Iliashibu Masatu – Mkuu wa utafiti
  4. Funk Kiduku – mwanachama
  5. Meta Mkorofi – katibu
Waliotuma Udhuru
  1. Bahatika Mashauri – Naibu Mwenyekiti
  2. Ponea Kamgazi – Msimamizi wa Mijadala
Waliokosa Kuhudhuria
  1. Zebedayo Chisege – Spika
  2. John Kumbikumbi – mwanachama
Waalikwa
  1. Mnoko Nokwe – Mwanahabari
  2. Dkt. Fikirini– Mlezi wa Chama.
Ajenda
  1. Uchapishaji wa jarida la Kiswahili
  2. Shindano la kuandika insha.
  3. Kusajili wanachama wapya

KUMBUKUMBU 3/04/14 – KUFUNGULIWA KWA MKUTANO
Mwenyekiti aliwakaribisha wanachama wote na baada ya kuwatambulisha wageni, akawaomba washiriki wawe huru kuchangia katika ajenda mkutano huu ili kuboresha chama.

KUMBUKUMBU 7/04/14 – KUREJELEA KUMBUKUMBU ZA MKUTANO ULIOPITA
Katibu alisoma kumbukumbu za mkutano wa mwezi Machi. Kumbukumbu zilikubaliwa na wanachama wote na kuthibitishwa na mwenyekiti pamoja na katibu kwa kutia saini.

KUMBUKUMBU 10/04/14 – MASWALA IBUKA KUTOKANA NA KUMBUKUMBU ZILIZOSOMWA
Mweka hazina alifahamisha mkutano kwamba aliongea na mkuu wa idara ya Kiswahili kuhusu ufadhili kama tulivyokuwa tumekubaliana katika KUMB 9/03/10 ya mkutano uliopita.

KUMBUKUMBU 12/04/14 – HAFLA YA KISWAHILI
Iliripotiwa kwamba hafla ya Kiswahili ambayo wanachama walikuwa wamealikwa kuhudhuria katika Shule ya Sakata Academy haingeweza kufanyika kutokana na tamasha la muziki lilizokuwa linaendelea katika shule hiyo. Wanachama waliokuwa wamejitayarisha kwa mashairi waliombwa kuendelea kujifunza ili wayawasilishe muhula wa pili.

KUMBUKUMBU 15/04/14 – UCHAPISHAJI WA JARIDA LA KISWAHILI
Wanachama walikubaliana:
  • Kwamba chama kitaanza kuchapisha jarida la Kiswahili
  • Kwamba jarida litakuwa likichapishwa mara moja kila muhula na kuuzwa shuleni
  • Kwamba kila mwanachama atachangia katika kuandika makala na kuuza nakala za jarida hilo.
  • Kwamba paneli ya wahariri lingeundwa ili kuongoza idara ya uchapishaji
  • Kwamba hazina ya chama ina fedha za kutosha kuzindua uchapishaji huo.

KUMBUKUMBU 17/04/14 – SHINDANO LA KUANDIKA INSHA
Kila muhula wa pili, chama huandaa shindano la kuandika insha ambalo wanafunzi wote hushiriki. Insha zilizopendekezwa mwaka huu ni:
  • “Jadili chanzo cha migomo shuleni na namna ya kusuluhisha.”
  • … … … … … … … … …
  • … … … … … … … … …
  • … … … … … … … … …

KUFUNGWA KWA MKUTANO
Mkutano ulifungwa saa kumi na nusu, baada ya maswala yote kujadiliwa. Mkutano unaofuatia ulipoangwa kuwa tarehe ishirini mwezi Mei, katika Ukumbi wa Muziki.

KUTHIBITISHWA KWA KUMBUKUMBU
______________
_____________
Mwenyekiti
Katibu
Tarehe:________
Tarehe:________









EmoticonEmoticon