Close Menu
Msomi BoraMsomi Bora
    Facebook X (Twitter) Instagram Threads WhatsApp
    Msomi BoraMsomi Bora
    • HOME
    • NOTES
    • PAST PAPERS
    • BOOKS
    • OTHERS
    • KENYA
    • CONTACT US
    Msomi BoraMsomi Bora
    Home»Kiswahili»KISWAHILI: FORM THREE: Topic 4 – UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
    Kiswahili

    KISWAHILI: FORM THREE: Topic 4 – UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

    June 23, 20189 Mins Read
    Facebook Twitter Pinterest LinkedIn WhatsApp

    JOIN US WHATSAPP CLICK HERE
    JOIN US TELEGRAM CLICK HERE

    TOPIC
    4:
    UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

    Fasihi
    andishi ni tawi la fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa
    hadhira kwa njia ya maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa
    hizo ni pamoja na hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi.
    Maana ya Uhakiki
    Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu
    ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana kwamba
    uhakiki wa kazi za fasihi hautoki katika ombwe, kuna kanuni na taratibu mbalimbali
    zinazoongoza kufanya uhakiki, na hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha
    za uhakiki wa kazi za kifaishi. AU kwa lugha rahisi tunaweza kusema, uhakiki ni
    uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi
    kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.
    Misingi ya
    Uhakiki
    Kwa ujumla mhakiki wa kazi za fasihi anapofanya uhakiki wa kazi za
    kifasihi, huwa analenga vipengele viwili. Pengine analenga kuhakiki fani ya
    kazi husika au maudhui ya kazi hiyo na wakati mwingine vyote viwili. Kwa
    hiyo kupitia vipengele hivi ndipo atachambua vitu vingi kama vile ujumbe,
    falsafa, matumizi ya lugha, dhamira, mandhari na kadhalika.
    Kuhakiki Fani
    Katika utunzi wa kazi za kifasihi, Fani hutumika kama nyezo ya kuwasilisha
    mawazo ya mwandishi kwa njia ya kisanaa zaidi. Fani ni mbinu anayoitumia
    mwandshi ili kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia.

    Vipengele vya fani ni pamoja na wahusika, mandhari, lugha, muundo na mtindo.

    Mtindo
    Mtindo ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii
    mmoja na mwingine. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua
    msamiati, namna anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi ya kwanza, ya
    pili au ya tatu). Kwa mfano katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” iliyoandikwa
    na Mariama Ba ametumia mtindo wa barua ya kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho,
    hii pia inaonesha mtindo wake wa kipekee.
    Muundo
    Muundo ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi
    yake. mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na matukio.
    Kuna aina mbili za kupangilia matukio
    1. Msago; hii ni namana ya moja kwa moja ya
    kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna
    yalivyotukia. Huu ni muundo wa moja kwa moja.
    2. Urejeshi; huu ni usimuliaji wa kurukaruka
    hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na
    mwanzo
    Wahusika
    Wahusika; ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili
    kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa
    wahusika katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.

    Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa
    kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu
    mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni
    mwa kitabu.

    Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika katika makundi
    yafuatayo:
    1. Mhusika mviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali
    halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya
    maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya
    na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
    2. Mhusika bapa ni mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano;
    kama ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama
    ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.
    3. Mhusika shinda yuko
    katikikati ya mhusika papa na mviringo. Huongozwa na matendo ya hao wahusika
    wawili. Hajitokezi na msimamo wake imara.
    Mandhari
    Mandhari; hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea.
    Mandhari huweza kuwa halisi kama vile baharini, njiani, msituni, kijijini,
    mijini au ya kufikirika kama vile kuzimu, mbinguni, peponi n.k.
    Lugha
    Lugha ndio nyenzo kubwa ya msanii katika kazi za fasihi, miongoni mwa
    vipengele vya lugha ni tamathali za semi pamoja na semi.

    Fani za Lugha
    1. Tanakali za Sauti: Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo
    kilivyofanyika.
    2. Tashbiha: Hii ni mbinu ya lugha
    inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha;
    ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano.
    3. Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia
    kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano,
    “Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi”.
    4. Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia
    neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia,
    alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.
    5. Ukinzani: Ukinzani ni mbinu ya
    kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
    6. Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha
    vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni
    mlima, juma ni mwamba.
    7. Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno
    yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
    8. Taashira: Ni matumizi ya lugha ya
    ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha
    kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
    9. Jazanda: Ni kulinganisha vitu viwili
    moja kwa moja bila kutumia viunganishi.
    10. Majazi: Majazi ni pale tabia za
    wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
    11. Lakabu: Ni mbinu ya mhusika
    kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina
    linalooana na tabia/sifa zake.
    12. Chuku: Ni kutumia maneno
    yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu, kutilia
    Chumvi.

    Semi
    Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya
    maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha.
    Kuna aina mbili za semi:
    – Nahau – ni usemi unaotumia maneno ya
    kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno
    hayo. Nahau huwa na vitenzi.
    – Misemo – ni semi fupifupi ambazo hutumiwa
    mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.
    1. Maswali ya Balagha: Tashititi au maswali ya balagha ni maswali yanayoulizwa na msimulizi
    au mhusika ambayo hayahitaji jibu.
    2. Uzungumzi Nafsiya: Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia
    kusikika na yeyote.
    3. Ritifaa: Mbinu ya kuzungumza na mtu
    aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.
    4. Kuchanganya Ndimi: Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili
    katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, “alisimama kwanza kwa muda, before he
    went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!”
    5. Kuhamisha Ndimi: Ni
    kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili.
    Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika
    sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine
    hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu. Mfano: Kazi hii ni ngumu
    sana, sitaweza kuifanya. People are trying to convince me to stay here but I
    think I can’t, I must go!
    6. Methali: Methali ni misemo ya hekima
    yenye maana iliyofumbwa. Mhusika, mwandishi wa fasihi anaweza kutumia methali
    kupitisha ujumbe.
    Mbinu nyingine za Kisanaa
    1. Kinaya: Kinaya ni mambo katika
    sanaa kuwa kinyume na matarajio ya hadhira.
    2. Kejeli; Kejeli ni mbinu ya sanaa
    inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani.
    3. Taharuki; Taharuki ni mbinu ya
    kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kufanya hadhira na/au wahusika wajawe
    na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea
    kusoma/kusikiliza. Baadhi ya hadithi huishia kwa taharuki na kuilazimisha
    hadhira yake ijikamilishie au ibaki ikijiuliza maswali.
    4. Sadfa; Sadfa ni kugongana kwa vitendo
    viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa, japo havikuwa
    vimepangiwa.
    5. Kisengere Nyuma; Mwandishi
    ‘hurudi nyuma’ na kuanza kusimulia kisa kilichokuwa kimetendeka kabla ya
    alichokuwa akisimulia. Aidha, mwandishi hubadilisha wakati wa masimulizi na kuwa
    wakati wa kisa hicho. Hutumika sana kuonyesha mhusika anapokumbuka kitu, au
    kutupatia msingi wa jinsi mambo yalivyoanza.
    6. Kisengere Mbele; Mwandishi
    anapobadilisha wakati na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni; au
    kutumia lugha isiyo moja kwa moja kutabiri yatakayojiri. Utabiri.
     

    Fasihi Andishi

    KUHAKIKI MAUDHUI
    Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa
    pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo
    pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi
    fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro,
    falsafa ujumbe na msimamo.
    1. Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo
    mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya
    maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira
    zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
    2. Migogoro; hii ni mivutano na
    misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika,
    familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile
    migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya
    kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa
    visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
    3. Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi
    yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika
    kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya
    fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira
    ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa
    msingi.
    4. Msimamo; katika kazi ya fasihi,
    mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala
    mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na
    kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini
    akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi
    wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano, katika tamthilia ya “Pesa
    zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo
    yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
    5. Falsafa ni mawazo ya busara yenye
    kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya
    mwanadamu. Ni msimamo wa msanii katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika
    jamii. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya
    moja.
    6. Mtazamo ni hisia au uelewa wa
    mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa mfano anaweza kutazama jambo fulani kwa
    mtazamo wa kidini, au anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kisiasa au
    kisayansi.
    7. Mafunzo; ni mawazo ya kuelimisha
    yanayopatikana katika dhamira mbalimbali za kazi ya fasihi.

    Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi
    Kufaulu au kutofaulu kwa mwandishi kunategemea jinsi alivyoweka uwiano
    mzuri kati ya fani na maudhui kwa namna ambavyo inaleta uhalisia. Mfano, endapo
    msanii atakuwa na mhusika Mkongo lakini akawa anazungumza kiswahili kilichojaa
    misemo na nahau alafu kimenyooka kama mtu wa pwani itakuwa vigumu kusema
    amefaulu kwani hakuna uwiano mzuri kati ya mhusika mwenyewe na lugha
    anayoitumia. Kiswahili cha Kongo ni tofauti kabisa na kiswahili
    kinachozungumzwa na watu wa pwani (Tanzania).

    Share. Facebook Twitter Pinterest LinkedIn WhatsApp
    Previous ArticleKISWAHILI: FORM THREE: Topic 3 – MAENDELEO YA KISWAHILI
    Next Article KISWAHILI: FORM THREE: Topic 5 – UTUNGAJI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

    Related Posts

    Uhakiki wa Tamthiliya | Form 5 and 6 | Advanced Level

    June 2, 2026

    Usaliti Mjini – Uhakiki wa Tamthiliya | Form 5 and 6

    June 2, 2026

    Shujaa Mirambo | Uhakiki wa Tamthiliya | Form 5 and 6

    June 2, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR FORM SIX – ALL TOPICS (Fasihi ya Kiswahili)

    May 6, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR FORM FIVE – ALL TOPICS (Lugha na Sarufi ya Kiswahili)

    May 6, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR ADVANCED LEVEL – Form 5 and 6

    May 6, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR FORM FOUR – ALL TOPICS

    May 6, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR FORM THREE – ALL TOPICS

    May 6, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR FORM TWO – ALL TOPICS

    May 6, 2026

    KISWAHILI NOTES FOR FORM ONE – ALL TOPICS

    May 6, 2026
    Clickable WP Image
    • Complaints
    • CONTACT US
    © 2026 Copyright. All Rights are Reserved. Msomi Bora.

    Type above and press Enter to search. Press Esc to cancel.